Friday 24 January 2014

SIKIO HALISI; JE UNATAKA KUBADILIKA KIFIKRA? UNGANA NAMI KATIKA

SIKIO HALISI Na, Gordon Kalulunga.
1.
JE UMEUMIZWA KIFIKRA NA MAISHA AU MWENZA WAKO NA UNATAKA KUBADILIKA NA UWE MTU MWENYE MAFANIKIO? UNGANA NAMI.
 
 
KAMA hatubadiliki, hatukui na kama hatukui basi tumekufa. 



Huo ndiyo ukweli katika maisha. Haya ni mafundisho ambayo yatakutoa hapo ulipo na kwenda sehemu tofauti na wengine.

Kama unataka kuendelea kuwa yule yule anayekosea, asiyejua kuomba radhi, asiyeweza kujiuliza maswali kuwa nini anatakiwa kufanya, hawezi kubadilika.

Tulio wengi hatutaki kukabiliana na mabadiliko, lakini kila siku tunafanya juhudi za kutaka kuwabadili wengine, wakati tunaendelea kufanya mambo yale yale.

Kuna kitabu niliwahi kukiona kimeandikwa hivi ‘’ kwanini mimi niwe wa kwanza kubadilika?’’ swali hili wengi wetu tunajiuliza bila kupata majibu.

Lakini nikuambie kuwa, ukiwa wa kwanza wewe kubadilika, utakuwa na furaha zaidi kama utaendelea kukua na kujifunza zaidi. 

Ukibadilika utaanza kuwajibika kwako wewe mwenyewe, yaani utawajibika kwa maisha yako kiutashi na nidhamu. 



Hivyo ukibadilika, watu wengine watabadilika na kukufuata, hii ni siri ninayokupa.

Lakini ni vema ukafahamu kuwa mabadiliko ni kitu kigumu sana ukizingatia ukweli kwamba, sisi binadamu ni viumbe wa tabia.

Na sehemu kubwa ya tabia zetu, tumefundishwa tangu utotoni, pamoja na tabia hizi, tunapaswa kubadilika ili kujua hasa maana ya maisha yetu.

Mabadiliko ni magumu kwasababu ya mazoea, hivyo njia moja kuu ya mabadiliko ni kutenda. Soma vitu ambavyo vinakubadilisha nk.

Kama huwezi kutenda hautaweza kuwa na mabadiliko, maana kutenda ndiko kunaleta mabadiliko wala si kukariri mambo.

Ni vizuri kujua mambo, kuwa na maarifa lakini ni hekima kuyatumia maarifa hayo.

Kumbuka kuwa huwezi kubadilika kwenye maeneo yote kwa wakati mmoja, mfano ulevi, uzinzi, dharau nk. Anza na jambo moja.

Kikubwa ndugu yangu nikuambie kuwa, bila nidhamu na utashi ni vigumu sana kubadilika, maana mabadiliko ya aina yeyote, yanataka nidhamu ya hali ya juu sana.

Mabadiliko maana yake ni kutoka kwenye mazoea lakini bahati mbaya tulio wengi hatutaki kutoka kenye mazoea na kuthubutu.

Lakini mimi nakuambia kuwa inawezekana, Nchi kama china na nyinginezo, jamii zao ziliumia mfumo ulipobadilika, sasa jiulize kuwa je kama jamii inaweza kuumia wakati wa mabadiliko sembuse wewe mmoja katika mabadiliko ya maisha yako? Anza sasa. 

Je unataka kuanza kubadilika kwenye hasira, fitina au ipi? Kusikia ni chanzo cha maarifa, bila shaka umenisikia kupitia sikio hili halisi.

Tunakuwa na masomo haya ya sikio halisi kwa wale wanaohitaji kwenye kumbi mbalimbali nchini, kwa sasa tupo mkoani Mbeya.

Wiki hii tutakuwa ukumbi wa Tughimbe Hotel Mbalizi Mbeya, kwa kiingilio cha Shilingi 5,000/=

Ni kuanzia saa Nane kamili mchana mpaka saa kumi jioni, nyote mnakaribishwa.



Tukutane wakati mwingine katika mafundisho haya.

Teta nami kwa SIMU; 0754 440749/0787552955

Email; kalulunga2006@gmail.com
WEB; www.kalulunga.com
Wenu katika sikio halisi

Gordon Kalulunga.
 
 

LEO TENA KATIKA MFULULIZO WA.....

SIKIO HALISI

2.
KUNA hadithi niliyowahi kusimuliwa, ambayo wakati ule sikuielewa maana yake kutokana na umri wangu wa wakati huo.
Lakini leo hii ninao uwezo wa kuieleza na kuitumia katika sikio lako halisi ambalo linaweza kukupelekea mabadiliko, je unataka kuisikiliza na upo tayari kubadilika? basi ungana nami tena leo.

Hapo zamani kulikuwa na mfalme mwenye akili sana ambaye siku moja aliamua kupima ufahamu wa watu wake kuhusiana na maisha.

Aliwatuma wasaidizi wake kwenda kuweka jiwe kubwa katikati ya barabara, wasaidizi wake walifanya hivyo huku yeye akijificha kwenye kichaka ambacho kilikuwa karibu na barabara hiyo.

Alifanya vile ili aweze kuona ni nani ambaye angeweza kuliondoa jiwe lile.

Watu mbalimbali walipita mahala pale na kulikwepa jiwe na kupita pembeni ya barabara. 

Wengine walipofika pale walilaumu sana na kusema huyu mfalme pamoja na utawala wake ameshindwa kuondoa jiwe lile katikati ya barabara, na kusema kuwa, kuna wafalme wengine hawafai, maana wapo kwenye madaraka lakini hawawezi kuwasaidia.

Ni kama maumbile kwa watu kulaumu mamlaka endapo jambo halijafanyika bila kujali mazingira. 

Walipita wasomi, matajiri na wananchi wa kila namna huku wakikwepa lile jiwe.

Hatimaye kuna mkulima mmoja, mahali pale akiwa na mzigo wa mboga kichwani na kuanza kulitizama lile jiwe kwa muda.

Kisha alitua mzigo wake na kuliendela na kuanza juhudi za kulisukuma kulitoa mahala pale, alijitahidi sana kwasababu jiwe lilikuwa kubwa na yeye alikuwa peke yake.

Alitumia muda mrefu sana kulisukuma lile jiwe, na hatimaye lile jiwe likasogea pembeni mwa barabara. 

Wakati akirudi kwenda kuichukua mboga yake, aliona pochi mahala pale lilipokuwepo jiwe! 

Akaiendela na kukuta pochi ile imejaa vipande vya dhahabu vikubwa na vingi.

Mkulima yule akarejea nyumani akiwa tajiri mkubwa. 
Hadithi hii ina mafunzo kwamba ni vizuri mtu au watu tukawa na moyo wa kujitolea kwa ajili yetu na kwa ajili ya wengine.

Yule mtu hakutarajia kama angeweza kupata pochi endapo angesukuma lile jiwe, lakini kwasababu alikuwa na moyo wa kujitolea ndiyo maana akapata mafanikio. Hivyo kwa wakati mwingine kujitolea kunalipa.

Kama kila kitu unataka kupata pesa, inaweza kula kwako maana kwenye maisha hatupaswi kukwepa vizuizi.
Tunapokutana na vizuizi kwenye nia zetu za kuelekea kupata mafanikio, hatupaswi kuvikwepa maana hivyo siyo vizuizi bali ni taarifa ya kwamba mbele kuna mafanikio na dhahabu.
Kwa kuhofia vizuizi na shida zinazotukabili katika maisha yetu, tunajikuta tunashindwa kupata dhahabu na mali au vitu vya thamani.

Kwa bahati mbaya kila mmoja wetu, bila kujali nafasi yake katika jamii, anaogopa kizuizi na kila mmoja anatamani mwenzake apambane na kizuizi na siyo yeye.

Sikiliza nikueleze, ni wazi kuwa kila palipo na kizuizi, ndipo palipo na njia nzuri ya kupita na kupata mafanikio.


Tukiwa na moyo wa kupenda kujitolea na moyo wa kutokwepa vikwazo vya kimasha ndipo tutakuwa na uwezo wa kupata mafanikio tunayoyataka.

Usijaribu kukwepa ukweli na kuanza kunywa pombe eti unataka kujisahaulisha na usidhani kuwa ni wajibu wa mtu mwingine kubadili hali uliyonayo kufikia mafanikio.

Bali ni wajibu na jukumu lako kuhakikisha kwamba, njia ikifungwa, unajitahidi kuifungua.

Hata ukilaumu kwa miaka mingi kiasi gani, bado vikwazo vitaendelea kuwepo endapo hautataka kuvikabili.
Tujifunze kwa yule mkulima wa mboga, ambaye hakuamua kuanza kumlaumu mtu, bali aliamua kutua mboga zake na kwenda kulisukuma jiwe hatimaye akapata mafanikio.

Kuna wenye njaa na matajiri na wengine waliopita pale, hawakuona kuwa ni jukumu lao kuondoa lile jiwe bali ni jukumu la serikali, au watu wajinga! Badala yake kumbe walikuwa wakikwepa mafanikio.

Kuna watu wamefeli shule na wengine kwenye mahusiano mambo yameenda ndivyo sivyo, wanadhani wameachwa na Mungu. Lakini katika kikwazo hicho kuna kitu kimejificha cha mafanikio.

Mafundisho haya pia tunayatoa kwa njia ya mikutano katika kumbi mbalimbali nchini Tanzania kwa kualikwa ama kuandaa wenyewe mikutano hiyo kwa kiingilio kidogo kabisa.

Tukutane wakati mwingine katika mafundisho haya. 
Kama una jambo lolote ama unataka kutualika popote, 
Teta nasi kwa SIMU; 0754 440749/0787552955
Email; kalulunga2006@gmail.com
WEB; www.kalulunga.com
Wenu katika sikio halisi
Gordon Kalulunga.
 
 
3.
SIKIO HALISI Na, Gordon Kalulunga.
Tumia matatizo yako kupata mafanikio au kujididimiza zaidi.
Mungu anataka kilakitu unachotaka uwe nacho hapa duniani, ukipate.
Hivi ndivyo nilivyowahi kuambiwa miaka ya nyuma kidogo.
Haikuwa rahisi kuamini kuwa maneno hayo yalikuwa na nguvu ya kuweza kubadili maisha yangu.
Siku moja nilijiuliza moyoni kuwa kwanini Mungu hakutaka niwe kama wenzangu ambao wana nyumba nzuri na magari mazuri nk.
Lakini sikupata jibu! Nikaiambia nafsi yangu kuwa je mimi nina laana? Je Mungu ana upendeleo? Mbona watu wanasema Mungu hana upendeleo?
Nilizidi kuwaza, huku baadhi wakinikejeli! Mawazo yakanizidi kichwani.
Kuna siku nikawa naelekea mjini, wakati navuka barabara nikiwa na lindi la mawazo huku nikijihisi mtupu, niliponea chupuchupu kufa kwa kugongwa na gari.
Dereva yule alinikwepa kisha akasimamisha gari na kuaza kunitukana sana matusi ya nguoni, na kunitolea maneno makali ya kashfa, hakika yalinichoma sana moyoni.
Nikaanza kuhisi kuwa nina mkosi zaidi, mtu ambaye sina bahati na hatimaye machozi yakanidondoka huku nikiendelea kutembea.
Ukiona mwanaume analia basi kuna jambo! Ghafla nikaona lile gari lililotaka kunigonga, likinifuata tena kwa kasi! Na yule dereva akaniambia anipe rifti.
Nikakubali kwa shingo upande na nikiwa ndani ya gari, dereva akaniuliza kama kuna jambo limenikuta, kwani alihisi nina mawazo sana.
Nikavuta pumzi na kumwambia. Ndipo naye akaniambia kuwa, kuna siku moja Ng’ombe wake alitumbukia ndani ya shimo refu na akajaribu kumtoa lakini akashindwa.
Baadhi ya majirani zake ambao hawakumpenda na kupenda mafanikio yake walifurahi sana na wakaanza kutupa matakataka na udongo ndani ya shimo ili kumdhuru yule Ng’ombe afe.
Alisema wakati akiwa kazini, wabaya wake hao, walipokuwa wakitupa takataka hizo na udongo, bila kujua, kumbe yule Ng’ombe alikuwa akijikung’uta zile takataka na udongo ukawa unashuka chini yeye anakanyaga na kupanda juu.
Kadri walivyozidi mumtupia takataka na udongo, akazidi kupanda! Kufumba na kufumbua, yule Ng’ombe akatokeza kichwa na kulia Mmoooooo!
Watu walitaaruki, kuwa iweje Ng’ombe yule katoka mzima! Ndipo yule dereva aliponiambia kuwa, kuna wakati inafikia kila aina ya uchafu utatupiwa, lakini ni maamuzi yako kuamua kijikung’uta na kutumia uchafu huo huo kama daraja la kukuvusha nje au ukubali kufunikwa na huo uchafu kisha ufe.
Maneno ya dereva huyu, yanatukumbusha kuwa kuna wakati wa kulia na wakati wa kucheka,  pia kuna wakati wa kupada na wakati wa kuvuna.
Sikiliza nikuambie, unaweza kuinuka tena, sikio lako halisi naamini limesikia.
 Tukutane wakati mwingine katika mafundisho haya.

Teta nami kwa SIMU; 0754 440749/0787552955

Email; kalulunga2006@gmail.com
WEB; www.kalulunga.com
Wenu katika sikio halisi

Gordon Kalulunga.

No comments:

Post a Comment