SIKIO HALISI Na,
Gordon Kalulunga.
1.
JE UMEUMIZWA KIFIKRA NA MAISHA AU MWENZA WAKO NA UNATAKA KUBADILIKA NA UWE MTU MWENYE MAFANIKIO? UNGANA NAMI.
KAMA
hatubadiliki, hatukui na kama hatukui basi tumekufa.
Huo ndiyo ukweli katika
maisha. Haya ni mafundisho ambayo yatakutoa hapo ulipo na kwenda sehemu tofauti
na wengine.
Kama unataka
kuendelea kuwa yule yule anayekosea, asiyejua kuomba radhi, asiyeweza kujiuliza
maswali kuwa nini anatakiwa kufanya, hawezi kubadilika.
Tulio wengi
hatutaki kukabiliana na mabadiliko, lakini kila siku tunafanya juhudi za kutaka
kuwabadili wengine, wakati tunaendelea kufanya mambo yale yale.
Kuna kitabu
niliwahi kukiona kimeandikwa hivi ‘’ kwanini mimi niwe wa kwanza kubadilika?’’
swali hili wengi wetu tunajiuliza bila kupata majibu.
Lakini
nikuambie kuwa, ukiwa wa kwanza wewe kubadilika, utakuwa na furaha zaidi kama
utaendelea kukua na kujifunza zaidi.
Ukibadilika
utaanza kuwajibika kwako wewe mwenyewe, yaani utawajibika kwa maisha yako
kiutashi na nidhamu.
Hivyo ukibadilika, watu wengine watabadilika na kukufuata,
hii ni siri ninayokupa.
Lakini ni
vema ukafahamu kuwa mabadiliko ni kitu kigumu sana ukizingatia ukweli kwamba,
sisi binadamu ni viumbe wa tabia.
Na sehemu
kubwa ya tabia zetu, tumefundishwa tangu utotoni, pamoja na tabia hizi,
tunapaswa kubadilika ili kujua hasa maana ya maisha yetu.
Mabadiliko
ni magumu kwasababu ya mazoea, hivyo njia moja kuu ya mabadiliko ni kutenda.
Soma vitu ambavyo vinakubadilisha nk.
Kama huwezi
kutenda hautaweza kuwa na mabadiliko, maana kutenda ndiko kunaleta mabadiliko
wala si kukariri mambo.
Ni vizuri
kujua mambo, kuwa na maarifa lakini ni hekima kuyatumia maarifa hayo.
Kumbuka kuwa
huwezi kubadilika kwenye maeneo yote kwa wakati mmoja, mfano ulevi, uzinzi,
dharau nk. Anza na jambo moja.
Kikubwa
ndugu yangu nikuambie kuwa, bila nidhamu na utashi ni vigumu sana kubadilika,
maana mabadiliko ya aina yeyote, yanataka nidhamu ya hali ya juu sana.
Mabadiliko
maana yake ni kutoka kwenye mazoea lakini bahati mbaya tulio wengi hatutaki
kutoka kenye mazoea na kuthubutu.
Lakini mimi
nakuambia kuwa inawezekana, Nchi kama china na nyinginezo, jamii zao ziliumia
mfumo ulipobadilika, sasa jiulize kuwa je kama jamii inaweza kuumia wakati wa
mabadiliko sembuse wewe mmoja katika mabadiliko ya maisha yako? Anza sasa.
Je unataka
kuanza kubadilika kwenye hasira, fitina au ipi? Kusikia ni chanzo cha maarifa,
bila shaka umenisikia kupitia sikio hili halisi.
Tunakuwa na
masomo haya ya sikio halisi kwa wale wanaohitaji kwenye kumbi mbalimbali nchini, kwa
sasa tupo mkoani Mbeya.
Wiki hii
tutakuwa ukumbi wa Tughimbe Hotel Mbalizi Mbeya, kwa kiingilio cha Shilingi
5,000/=
Ni kuanzia
saa Nane kamili mchana mpaka saa kumi jioni, nyote mnakaribishwa.
Tukutane wakati mwingine katika mafundisho haya.
Teta nami
kwa SIMU; 0754 440749/0787552955
Email; kalulunga2006@gmail.com
WEB; www.kalulunga.com
Wenu katika
sikio halisi
Gordon
Kalulunga.
2.
KUNA hadithi
niliyowahi kusimuliwa, ambayo wakati ule sikuielewa maana yake kutokana na umri
wangu wa wakati huo.
Lakini leo
hii ninao uwezo wa kuieleza na kuitumia katika sikio lako halisi ambalo
linaweza kukupelekea mabadiliko, je unataka kuisikiliza na upo tayari kubadilika? basi ungana nami tena leo.
Hapo zamani
kulikuwa na mfalme mwenye akili sana ambaye siku moja aliamua kupima ufahamu wa
watu wake kuhusiana na maisha.
Aliwatuma
wasaidizi wake kwenda kuweka jiwe kubwa katikati ya barabara, wasaidizi wake
walifanya hivyo huku yeye akijificha kwenye kichaka ambacho kilikuwa karibu na
barabara hiyo.
Alifanya
vile ili aweze kuona ni nani ambaye angeweza kuliondoa jiwe lile.
Watu
mbalimbali walipita mahala pale na kulikwepa jiwe na kupita pembeni ya barabara.
Wengine walipofika
pale walilaumu sana na kusema huyu mfalme pamoja na utawala wake
ameshindwa kuondoa jiwe lile katikati ya barabara, na kusema kuwa, kuna
wafalme wengine
hawafai, maana wapo kwenye madaraka lakini hawawezi kuwasaidia.
Ni kama
maumbile kwa watu kulaumu mamlaka endapo jambo halijafanyika bila kujali
mazingira.
Walipita wasomi, matajiri na wananchi wa kila namna huku wakikwepa
lile jiwe.
Hatimaye
kuna mkulima mmoja, mahali pale akiwa na mzigo wa mboga kichwani na kuanza
kulitizama lile jiwe kwa muda.
Kisha alitua
mzigo wake na kuliendela na kuanza juhudi za kulisukuma kulitoa mahala pale,
alijitahidi sana kwasababu jiwe lilikuwa kubwa na yeye alikuwa peke yake.
Alitumia
muda mrefu sana kulisukuma lile jiwe, na hatimaye lile jiwe likasogea pembeni
mwa barabara.
Wakati akirudi kwenda kuichukua mboga yake, aliona pochi mahala
pale lilipokuwepo jiwe!
Akaiendela na kukuta pochi ile imejaa vipande vya
dhahabu vikubwa na vingi.
Mkulima yule
akarejea nyumani akiwa tajiri mkubwa.
Hadithi hii ina mafunzo kwamba ni vizuri
mtu au watu tukawa na moyo wa kujitolea kwa ajili yetu na kwa ajili ya wengine.
Yule mtu
hakutarajia kama angeweza kupata pochi endapo angesukuma lile jiwe, lakini
kwasababu alikuwa na moyo wa kujitolea ndiyo maana akapata mafanikio. Hivyo kwa
wakati mwingine kujitolea kunalipa.
Kama kila
kitu unataka kupata pesa, inaweza kula kwako maana kwenye maisha hatupaswi
kukwepa vizuizi.
Tunapokutana
na vizuizi kwenye nia zetu za kuelekea kupata mafanikio, hatupaswi kuvikwepa
maana hivyo siyo vizuizi bali ni taarifa ya kwamba mbele kuna mafanikio na
dhahabu.
Kwa kuhofia
vizuizi na shida zinazotukabili katika maisha yetu, tunajikuta tunashindwa
kupata dhahabu na mali au vitu vya thamani.
Kwa bahati
mbaya kila mmoja wetu, bila kujali nafasi yake katika jamii, anaogopa kizuizi
na kila mmoja anatamani mwenzake apambane na kizuizi na siyo yeye.
Sikiliza
nikueleze, ni wazi kuwa kila palipo na kizuizi, ndipo palipo na njia nzuri ya
kupita na kupata mafanikio.
Tukiwa na
moyo wa kupenda kujitolea na moyo wa kutokwepa vikwazo vya kimasha ndipo
tutakuwa na uwezo wa kupata mafanikio tunayoyataka.
Usijaribu
kukwepa ukweli na kuanza kunywa pombe eti unataka kujisahaulisha na usidhani
kuwa ni wajibu wa mtu mwingine kubadili hali uliyonayo kufikia mafanikio.
Bali ni
wajibu na jukumu lako kuhakikisha kwamba, njia ikifungwa, unajitahidi
kuifungua.
Hata
ukilaumu kwa miaka mingi kiasi gani, bado vikwazo vitaendelea kuwepo endapo
hautataka kuvikabili.
Tujifunze
kwa yule mkulima wa mboga, ambaye hakuamua kuanza kumlaumu mtu, bali aliamua
kutua mboga zake na kwenda kulisukuma jiwe hatimaye akapata mafanikio.
Kuna wenye njaa
na matajiri na wengine waliopita pale, hawakuona kuwa ni jukumu lao kuondoa lile jiwe bali
ni jukumu la serikali, au watu wajinga! Badala yake kumbe walikuwa wakikwepa
mafanikio.
Kuna watu
wamefeli shule na wengine kwenye mahusiano mambo yameenda ndivyo sivyo, wanadhani
wameachwa na Mungu. Lakini katika kikwazo hicho kuna kitu kimejificha cha
mafanikio.
Mafundisho
haya pia tunayatoa kwa njia ya mikutano katika kumbi mbalimbali nchini
Tanzania kwa kualikwa ama kuandaa wenyewe mikutano hiyo kwa kiingilio
kidogo kabisa.
Tukutane wakati mwingine katika mafundisho haya.
Kama una jambo lolote ama unataka kutualika popote,
Teta nasi
kwa SIMU; 0754 440749/0787552955
Email; kalulunga2006@gmail.com
WEB; www.kalulunga.com
Wenu katika
sikio halisi
Gordon
Kalulunga.
3.
SIKIO HALISI Na,
Gordon Kalulunga.
Tumia
matatizo yako kupata mafanikio au kujididimiza zaidi.
Mungu
anataka kilakitu unachotaka uwe nacho hapa duniani, ukipate.
Hivi ndivyo
nilivyowahi kuambiwa miaka ya nyuma kidogo.
Haikuwa rahisi kuamini kuwa maneno
hayo yalikuwa na nguvu ya kuweza kubadili maisha yangu.
Siku moja
nilijiuliza moyoni kuwa kwanini Mungu hakutaka niwe kama wenzangu ambao wana
nyumba nzuri na magari mazuri nk.
Lakini
sikupata jibu! Nikaiambia nafsi yangu kuwa je mimi nina laana? Je Mungu ana
upendeleo? Mbona watu wanasema Mungu hana upendeleo?
Nilizidi kuwaza,
huku baadhi wakinikejeli! Mawazo yakanizidi kichwani.
Kuna siku
nikawa naelekea mjini, wakati navuka barabara nikiwa na lindi la mawazo huku
nikijihisi mtupu, niliponea chupuchupu kufa kwa kugongwa na gari.
Dereva yule
alinikwepa kisha akasimamisha gari na kuaza kunitukana sana matusi ya nguoni,
na kunitolea maneno makali ya kashfa, hakika yalinichoma sana moyoni.
Nikaanza
kuhisi kuwa nina mkosi zaidi, mtu ambaye sina bahati na hatimaye machozi
yakanidondoka huku nikiendelea kutembea.
Ukiona
mwanaume analia basi kuna jambo! Ghafla nikaona lile gari lililotaka kunigonga,
likinifuata tena kwa kasi! Na yule dereva akaniambia anipe rifti.
Nikakubali
kwa shingo upande na nikiwa ndani ya gari, dereva akaniuliza kama kuna jambo
limenikuta, kwani alihisi nina mawazo sana.
Nikavuta
pumzi na kumwambia. Ndipo naye akaniambia kuwa, kuna siku moja Ng’ombe wake
alitumbukia ndani ya shimo refu na akajaribu kumtoa lakini akashindwa.
Baadhi ya
majirani zake ambao hawakumpenda na kupenda mafanikio yake walifurahi sana na
wakaanza kutupa matakataka na udongo ndani ya shimo ili kumdhuru yule Ng’ombe
afe.
Alisema
wakati akiwa kazini, wabaya wake hao, walipokuwa wakitupa takataka
hizo na udongo, bila kujua, kumbe yule Ng’ombe alikuwa akijikung’uta zile
takataka na udongo ukawa unashuka chini yeye anakanyaga na kupanda juu.
Kadri
walivyozidi mumtupia takataka na udongo, akazidi kupanda! Kufumba na kufumbua,
yule Ng’ombe akatokeza kichwa na kulia Mmoooooo!
Watu
walitaaruki, kuwa iweje Ng’ombe yule katoka mzima! Ndipo yule dereva
aliponiambia kuwa, kuna wakati inafikia kila aina ya uchafu utatupiwa, lakini
ni maamuzi yako kuamua kijikung’uta na kutumia uchafu huo huo kama daraja la
kukuvusha nje au ukubali kufunikwa na huo uchafu kisha ufe.
Maneno ya
dereva huyu, yanatukumbusha kuwa kuna wakati wa kulia na wakati wa
kucheka, pia kuna wakati wa kupada na
wakati wa kuvuna.
Sikiliza
nikuambie, unaweza kuinuka tena, sikio lako halisi naamini limesikia.
Tukutane wakati mwingine katika mafundisho haya.
Teta nami
kwa SIMU; 0754 440749/0787552955
Email; kalulunga2006@gmail.com
WEB; www.kalulunga.com
Wenu katika
sikio halisi
Gordon
Kalulunga.